Yehoahazi Mfalme Wa Israeli
1Katika mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wa Yoashi mwana wa Ahazia mfalme wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala Israeli katika Samaria, naye akatawala miaka kumi na saba. 2Akafanya maovu machoni pa Bwana kwa kufuata dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, na wala hakuziacha. 3Kwa hiyo hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Israeli na kwa muda mrefu akawaweka chini ya utawala wa Hazaeli mfalme wa Aramu, na Ben-Hadadi mwanawe.
4Ndipo Yehoahazi akamsihi Bwana rehema, naye Bwana akamsikiliza, kwa maana aliona jinsi mfalme wa Aramu alivyokuwa akiwatesa Israeli vikali. 5Bwana akamtoa mwokozi kwa ajili ya Israeli, nao wakaokoka kutoka kwenye mamlaka ya Aramu. Hivyo Waisraeli wakaishi katika nyumba zao wenyewe kama ilivyokuwa hapo awali. 6Lakini hawakuziacha dhambi za nyumba ya Yeroboamu, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda, bali wakaendelea kuzitenda. Nguzo ya Ashera pia iliendelea kusimama katika Samaria.
7Hapakubaki kitu chochote katika jeshi la Yehoahazi isipokuwa wapanda farasi hamsini, magari kumi ya vita na askari wa miguu elfu kumi, kwa kuwa mfalme wa Aramu alikuwa amewaangamiza hao wengine na kuwafanya kama mavumbi wakati wa kupura nafaka.
8Matukio mengine ya utawala wa Yehoahazi yote aliyoyafanya na mafanikio yake, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 9Yehoahazi akalala pamoja na baba zake, akazikwa huko Samaria. Naye Yehoashi mwanawe akawa mfalme baada yake.


