Tumefanywa Kuwa Hai Ndani Ya Kristo

1Kwa habari zenu, mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu, 2ambazo mlizitenda mlipofuatisha namna ya ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii. 3Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu, kama mtu mwingine yeyote. 4Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema. 6Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu, 7ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu. 8Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.