Pigo La Tano: Vifo Vya Mifugo
1Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo Bwana, Mungu wa Waebrania asemalo: “Waachie watu wangu waende ili wapate kuniabudu.” 2Kama ukikataa kuwaachia waende, nawe ukiendelea kuwashikilia, 3mkono wa Bwana utaleta pigo baya kwa mifugo yako, juu ya farasi wako, punda, ngamia, ngʼombe wako, kondoo na mbuzi. 4Lakini Bwana ataweka tofauti kati ya mifugo ya Israeli na ile ya Misri, kwamba hakuna mnyama wa Mwisraeli atakayekufa.’ ”
5Bwana akaweka wakati na kusema, “Kesho Bwana atalitenda hili katika nchi.” 6Siku iliyofuata Bwana akalitenda: Mifugo yote ya Wamisri ikafa, lakini hakuna hata mnyama mmoja wa wana wa Israeli aliyekufa. 7Farao akatuma watu kuchunguza, nao wakakuta kuwa hakuna hata mnyama mmoja wa Waisraeli aliyekufa. Lakini moyo wa Farao haukukubali kuwaachia watu waende.


