Unabii Dhidi Ya Amoni
1Neno la Bwana likanijia kusema: 2“Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Waamoni utabiri dhidi yao. 3Waambie, ‘Sikieni neno la Bwana Mwenyezi. Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ulisema, “Aha!” juu ya mahali pangu patakatifu palipotiwa unajisi, na juu ya nchi ya Israeli ilipoangamizwa, na juu ya watu wa Yuda walipokwenda uhamishoni, 4kwa hiyo nitawatia mikononi mwa watu wa mashariki mkawe mali yao. Watapiga kambi zao katikati yenu na kufanya makazi miongoni mwenu, watakula matunda yenu na kunywa maziwa yenu. 5Nitaufanya mji wa Raba kuwa malisho ya ngamia na Amoni kuwa mahali pa kondoo pa kupumzikia. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana. 6Kwa kuwa hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa umepiga makofi yako na kufanya kishindo kwa miguu, mkifurahia kwa mioyo yenu miovu juu ya yale mabaya yaliyoipata nchi ya Israeli, 7hivyo nitaunyoosha mkono wangu dhidi yako na kukutoa kuwa nyara kwa mataifa. Nitakukatilia mbali kutoka kwenye mataifa na kukungʼoa katika nchi. Nitakuangamiza, nawe utajua ya kuwa Mimi ndimi Bwana.’ ”


