14Ndipo Labani akamwambia, “Wewe ni nyama yangu na damu yangu mwenyewe.”
Yakobo Awaoa Lea Na Raheli
Baada ya Yakobo kukaa kwa Labani mwezi mzima, 15Labani akamwambia, “Kwa vile wewe ni jamaa yangu, ndiyo sababu unifanyie kazi bila ujira? Niambie ujira wako utakuwa nini.”
16Labani alikuwa na binti wawili, binti mkubwa aliitwa Lea na binti mdogo aliitwa Raheli. 17Lea alikuwa na macho dhaifu, lakini Raheli alikuwa na umbo la kupendeza na mzuri wa sura. 18Yakobo akampenda Raheli, akamwambia Labani, “Nitakutumikia kwa miaka saba kwa ajili ya kumpata Raheli binti yako mdogo.”
19Labani akasema, “Ni bora zaidi nikupe Raheli kuliko kumpa mtu mwingine yeyote. Kaa pamoja na mimi hapa.” 20Kwa hiyo Yakobo akatumika miaka saba ili kumpata Raheli, lakini ilionekana kwake kama siku chache tu kwa sababu ya upendo wake kwa Raheli.
21Ndipo Yakobo akamwambia Labani, “Nipe mke wangu. Muda wangu umekamilika, nami nataka nikutane naye kimwili.”
22Basi Labani akaalika watu wote wa mahali pale na akafanya karamu.
23Lakini ilipofika jioni, akamchukua Lea binti yake akampa Yakobo, naye Yakobo akakutana naye kimwili. 24Naye Labani akamtoa Zilpa, mtumishi wake wa kike, kuwa mtumishi wa Lea, binti yake.
25Kesho yake asubuhi, Yakobo akagundua kuwa amepewa Lea! Basi Yakobo akamwambia Labani, “Ni jambo gani hili ulilonitendea? Nilikutumikia kwa ajili ya Raheli, sivyo? Kwa nini umenidanganya?”
26Labani akajibu, “Si desturi yetu kumwoza binti mdogo kabla ya kumwoza binti mkubwa. 27Maliza juma la arusi ya binti huyu, kisha pia nitakupa huyu binti mdogo, kwa kutumika miaka mingine saba.”
28Naye Yakobo akafanya hivyo. Akamaliza juma na Lea, kisha Labani akampa Raheli binti yake kuwa mke wake. 29Labani akamtoa Bilha mtumishi wake wa kike kwa Raheli ili kuwa mtumishi wake. 30Pia Yakobo akakutana na Raheli kimwili, naye akampenda Raheli zaidi kuliko Lea. Yakobo akamtumikia Labani kwa miaka mingine saba.


