Yefta Na Efraimu
1Watu wa Efraimu wakaita majeshi yao, wakavuka kwenda Zafoni, wakamwambia Yefta, “Kwa nini mmekwenda kupigana na Waamoni bila kutuita ili twende pamoja nawe? Basi tutaichoma moto nyumba yako, pamoja nawe ukiwa ndani yake.”
2Yefta akajibu, “Mimi na watu wangu tulikuwa na ugomvi mkubwa na Waamoni, hata ingawa niliwaita hamkuniokoa katika mkono wao. 3Nilipoona kuwa hamkunipa msaada nikauhatarisha uhai wangu na nikavuka kupigana na Waamoni. Naye Bwana akanipatia ushindi dhidi yao. Sasa kwa nini mnanijia leo ili kupigana nami?”
4Ndipo Yefta akakusanya watu wa Gileadi pamoja na kupigana na Efraimu. Wagileadi wakawashinda Efraimu, kwa kuwa Waefraimu walisema, “Ninyi Wagileadi ni watoro mliotoroka toka Efraimu na Manase.” 5Wagileadi wakaviteka vivuko vya Yordani dhidi ya hao Waefraimu, kisha ilikuwa yeyote yule aliyenusurika katika Efraimu aliposema, “Niache nivuke,” hao watu wa Gileadi walimuuliza, “Je wewe ni Mwefraimu?” Kama alijibu “Hapana,” 6walimwambia, “Sawa, sema ‘Shibolethi.’ ” Iwapo alitamka, “Sibolethi,” kwa sababu hakuweza kutamka hilo neno sawasawa, walimkamata na kumuua hapo kwenye vivuko vya Yordani. Waefraimu 42,000 waliuawa wakati huo.
7Yefta akawa mwamuzi wa Waisraeli kwa muda wa miaka sita. Basi Yefta akafa, akazikwa katika mmojawapo wa miji ya Gileadi.


