Kifo Cha Samsoni

23Basi viongozi wa Wafilisti wakakusanyika pamoja ili kutoa kafara kwa mungu wao Dagoni na kufanya karamu, wakisema, “Mungu wetu amemtia adui yetu Samsoni mikononi mwetu.”

24Watu walipomwona Samsoni wakamsifu mungu wao, wakisema:

“Sasa mungu wetu amemtia adui yetu

mikononi mwetu,

yule aliyeharibu nchi yetu

na kuwaua watu wengi miongoni mwetu.”

25Mioyo yao ilipokuwa imefurahishwa wakasema, “Mleteni Samsoni aje acheze ili tufurahi.” Basi wakamleta Samsoni kutoka mle gerezani naye akacheza mbele yao.

Wakamweka kati ya nguzo mbili. 26Samsoni akamwambia mtumishi aliyeshika mkono wake, “Niweke mahali ambapo ninaweza kuzigusa nguzo ambazo zinategemeza jengo ili nipate kuziegemea.” 27Basi lile jengo lilikuwa na wingi wa watu waume kwa wake; viongozi wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na kwenye sakafu ya juu walikuwepo watu 3,000 waume kwa wake, waliokuwa wakimtazama Samsoni wakati anacheza. 28Ndipo Samsoni akamwomba Bwana, akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, unikumbuke. Ee Mungu, nakusihi ukanitie nguvu mara hii moja tena, ili kwa tendo hili nipate kulipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili.” 29Ndipo Samsoni akazikaribia zile nguzo mbili za katikati ambazo lile jengo lilikuwa linazitegemea. Akazishika moja kwa mkono wa kuume na nyingine mkono wa kushoto. 30Samsoni akasema, “Nife pamoja na Wafilisti!” Ndipo akazisukuma zile nguzo kwa nguvu zake zote, lile jengo likaanguka juu ya viongozi na watu wote waliokuwamo mle ndani yake. Hivyo akawaua watu wengi wakati wa kufa kwake kuliko siku za uhai wake.

31Basi ndugu zake na jamaa yote ya baba yake wakateremka kwenda kumchukua. Wakampandisha na kumzika kati ya Sora na Eshtaoli kwenye kaburi la Manoa baba yake. Naye Samsoni alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini.