Jaribu La Pili La Ayubu
1Siku nyingine wana wa Mungu walikuja kujionyesha mbele za Bwana. Shetani naye akaja pamoja nao kujionyesha mbele zake. 2Bwana akamuuliza Shetani, “Umetoka wapi?”
Shetani akamjibu Bwana “Natoka kuzunguka pote duniani, nikitembea huku na huko humo.”
3Bwana akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, mtu asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Naye bado anadumisha uadilifu wake, ingawa ulinichochea dhidi yake, ili nimwangamize pasipo sababu.”
4Shetani akamjibu Bwana, “Ngozi kwa ngozi! Mwanadamu atatoa vyote alivyo navyo kwa ajili ya uhai wake. 5Lakini nyoosha mkono wako na kuipiga nyama yake na mifupa yake, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”
6Bwana akamwambia Shetani, “Vema sana, kwa hiyo, yeye yumo mikononi mwako, lakini lazima umwachie uhai wake.”
7Basi Shetani akatoka mbele za Bwana naye akampiga Ayubu kwa majipu mabaya tangu nyayo za miguu yake hadi utosi wa kichwa. 8Ndipo Ayubu akachukua kigae na kujikuna nacho huku akiketi kwenye majivu.
9Mke wake akamwambia, “Je, bado unashikamana na uadilifu wako? Mlaani Mungu nawe ukafe!”
10Akamjibu, “Unazungumza kama vile ambavyo mwanamke mpumbavu yeyote angenena. Je, tupokee mema mikononi mwa Mungu, nasi tusipokee na udhia?”
Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi katika kusema kwake.


