Malipo Kwa Ajili Ya Makosa

5Bwana akamwambia Mose, 6“Waambie Waisraeli, ‘Wakati mwanaume au mwanamke akimkosea mwenzake kwa njia yoyote, na kwa hivyo akawa si mwaminifu kwa Bwana, mtu huyo ana hatia, 7na ni lazima atubu dhambi aliyoifanya. Ni lazima atoe malipo kamili kwa ajili ya kosa lake, aongeze sehemu ya tano juu ya malipo hayo na kutoa yote kwa mtu aliyemkosea. 8Lakini ikiwa mtu huyo hana jamaa ya karibu ambaye malipo yanaweza kufanywa kwa ajili ya kosa, malipo yatakuwa mali ya Bwana, nayo ni lazima apewe kuhani, pamoja na kondoo dume ambaye anatumika kufanyia upatanisho kwa ajili yake. 9Matoleo yote matakatifu ya Waisraeli wanayoleta kwa kuhani yatakuwa yake. 10Kila kitu cha mtu kilichowekwa wakfu ni chake mwenyewe, lakini kile atoacho kwa kuhani kitakuwa cha kuhani.’ ”