Select a Verse

Kuanguka Kwa Mwanadamu

1Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao Bwana Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?”

2Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyoko bustanini, 3lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’ ”

4Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. 5Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

6Mwanamke alipoona ya kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma katika matunda yake, akala, pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, naye akala. 7Ndipo macho yao wote wawili yakafumbuliwa, wakajiona kwamba walikuwa uchi; hivyo wakashona majani ya mtini, wakajifunika.

8Ndipo yule mwanaume na mkewe, waliposikia sauti ya Bwana Mungu alipokuwa akitembea bustanini jioni, wakajificha kutoka mbele za Bwana Mungu katikati ya miti ya bustani. 9Lakini Bwana Mungu akamwita Adamu, “Uko wapi?”

10Naye akajibu, “Nilikusikia katika bustani nikaogopa kwa sababu nilikuwa uchi, hivyo nikajificha.”

11Mungu akamuuliza, “Ni nani aliyekuambia ya kuwa ulikuwa uchi? Je, umekula matunda ya mti niliokuamuru usile?”

12Adamu akasema, “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja nami alinipa sehemu ya tunda kutoka kwenye huo mti, nami nikala.”

13Ndipo Bwana Mungu akamuuliza mwanamke, “Ni nini hili ambalo umelifanya?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”

14Hivyo Bwana Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili,

“Umelaaniwa kuliko wanyama wote

wa kufugwa na wa porini!

Utatambaa kwa tumbo lako

na kula mavumbi

siku zote za maisha yako.

15Nami nitaweka uadui

kati yako na huyo mwanamke,

na kati ya uzao wako na wake,

yeye atakuponda kichwa,

nawe utamuuma kisigino.”

16Kwa mwanamke akasema,

“Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako;

kwa utungu utazaa watoto.

Tamaa yako itakuwa kwa mumeo

naye atakutawala.”

17Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’

“Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako,

kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo

siku zote za maisha yako.

18Itazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako,

nawe utakula mimea ya shambani.

19Kwa jasho la uso wako

utakula chakula chako

hadi utakaporudi ardhini,

kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo,

kwa kuwa wewe u mavumbi

na mavumbini wewe utarudi.”

20Adamu akamwita mkewe Eva, kwa kuwa atakuwa mama wa wote walio hai.

21Bwana Mungu akawatengenezea Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. 22Kisha Bwana Mungu akasema, “Sasa mtu huyu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya. Sharti asiruhusiwe kunyoosha mkono wake na kuchuma pia kutoka mti wa uzima akala, naye akaishi milele.” 23Hivyo Bwana Mungu akamfukuzia mbali kutoka Bustani ya Edeni, akalime ardhi ambamo alitolewa. 24Baada ya kumfukuzia mbali Adamu, Mungu akaweka makerubi mashariki ya Bustani ya Edeni, pamoja na upanga wa moto ukimulika huku na huko kulinda njia ya kuuendea mti wa uzima.