Select a Verse

Zaburi 110

Bwana Na Mfalme Wake Mteule

Zaburi ya Daudi.

1Bwana amwambia Bwana wangu:

“Keti mkono wangu wa kuume,

mpaka nitakapowafanya adui zako

kuwa mahali pa kuweka miguu yako.”

2Bwana ataeneza fimbo yako ya utawala yenye nguvu kutoka Sayuni;

utatawala katikati ya adui zako.

3Askari wako watajitolea kwa hiari

katika siku yako ya vita.

Ukiwa umevikwa fahari takatifu,

kutoka tumbo la mapambazuko

utapokea umande wa ujana wako.

4Bwana ameapa,

naye hatabadilisha mawazo yake:

“Wewe ni kuhani milele,

kwa mfano wa Melkizedeki.”

5Bwana yuko mkono wako wa kuume,

atawaponda wafalme siku ya ghadhabu yake.

6Atawahukumu mataifa, akilundika mizoga

na kuwaponda watawala wa dunia nzima.

7Atakunywa maji katika kijito kando ya njia,

kwa hiyo atainua kichwa chake juu.