Select a Verse

Zaburi 79

Maombi Kwa Ajili Ya Wokovu Wa Taifa

Zaburi ya Asafu.

1Ee Mungu, mataifa yameuvamia urithi wako,

wamelinajisi Hekalu lako takatifu,

wameifanya Yerusalemu kuwa magofu.

2Wametoa maiti za watumishi

kuwa chakula cha ndege wa angani

na nyama ya watakatifu wako

kwa wanyama wa nchi.

3Wamemwaga damu kama maji

kuzunguka Yerusalemu yote,

wala hakuna yeyote wa kuwazika.

4Tumekuwa kitu cha aibu kwa jirani zetu,

cha dharau na mzaha kwa wale wanaotuzunguka.

5Hata lini, Ee Bwana? Je, wewe utakasirika milele?

Wivu wako utawaka kama moto hadi lini?

6Mwaga ghadhabu yako kwa mataifa yasiyokukubali,

juu ya falme za hao wasioliitia jina lako,

7kwa maana wamemrarua Yakobo

na kuharibu nchi ya makao yake.

8Usituhesabie dhambi za baba zetu,

huruma yako na itujie hima,

kwa maana tu wahitaji mno.

9Ee Mungu Mwokozi wetu, utusaidie,

kwa ajili ya utukufu wa jina lako;

tuokoe na kutusamehe dhambi zetu

kwa ajili ya jina lako.

10Kwa nini mataifa waseme,

“Yuko wapi Mungu wenu?”

Mbele ya macho yetu,

dhihirisha kati ya mataifa

kwamba unalipiza kisasi damu iliyomwagwa

ya watumishi wako.

11Kilio cha huzuni cha wafungwa kifike mbele zako;

kwa nguvu za mkono wako

hifadhi wale waliohukumiwa kufa.

12Walipize jirani zetu mara saba vifuani mwao

aibu walizovurumisha juu yako, Ee Bwana.

13Ndipo sisi watu wako, kondoo wa malisho yako,

tutakusifu milele;

toka kizazi hadi kizazi

tutasimulia sifa zako.